JE, WAJUA KUWA MUDA UNAYOYOMA?
Mwanadamu anayo maswali mengi ya
kujiuliza kuhusu wakati anaoishi hapa duniani tangu kuzaliwa hadi umri alionao. Mtu mwenye akili na ufahamu lazima atajiuliza na kujitathimini
kuwa amefanya nini katika umri alionao akiwa ni kijana au mzee.
Kama tunavyojua ya kuwa muda unakwenda kasi sana na kadiri siku zinavyosogea ndivyo maisha ya mwanadamu yanavyoelekea ukingoni.
Kuna
wakati natafakari juu ya maisha yangu na muda nilionao hapa duniani na
kujiuliza maswali mengi kila iitwapo leo. Siku zinaenda, miaka inasogea
na majira hayasimami, ni kama ilivyo dunia inavyojizungusha katika
mhimili wake bila kupumzika tukapata kuuona usiku na mchana ndivyo muda
unavyosogea au unavyoyoyoma. Lazima nijiulize nimefanya nini katika umri
nilio nao tangu nimeanza kupata ufahamu aidha nimeutumia muda wangu kwa
faida au hasara. Ni vyema kutambua kuwa kila siku ni siku mpya na siku
hazifanani katika muda wa mwanadamu kuishi hapa duniani unapoamka
asubuhi sio kama jana bali umekuwa na umri mwingine na muda wako wa
kuishi unaendelea kupungua huenda na nguvu zako zinaendelea kupungua
kulingana na umri unavyosogea. Ni vyema ndugu yangu ukagundua kuwa tuna
muda mchache sana wa kuishi hapa duniani wakati jambo ambalo wengi
wetu tumelisahau na wakati mwingi tunahangaika tukisema tunatafuta
maisha tungali tunapoteza nguvu nyingi na muda bila kujua.
Basi
angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali
kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za
uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi
ya Bwana. Waefeso 5:15-17
Ni
vigumu mtu kugundua mapema kuwa anapoteza muda ila hilo linaonekana
mara tu anapoona umri umesogea na hakuna alichokifanya katika maisha
kinachoweza kumsaidia katika wakati nguvu zake zimeanza kupungua.
"Pale unapopata akili ndipo unagundua kuwa ulikuwa umepotea."
Mara
nyingi tunapoteza muda katika mambo yasiyo ya msingi au kuleta faida
kwenye maisha tunaacha kufanya mambo muhimu ya uzalishaji ambayo
yanaweza kutunufaisha katika maisha tunayoishi na kwa vizazi vyetu
vijavyo.
Kwa sababu ya ujinga na kukosa maarifa
tunaangamizwa kwa kutoielewa teknolojia inayokuwa kwa kasi katika dunia
ya sasa kwa sababu tunapumbazwa na mambo ambayo wengine wameyatengeneza
na kila siku yanawapa faida wakati sisi tunaangamia. "Watu wangu
wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; Hosea 4:6"
Kukosa
maarifa siyo kukosa mtaji wala siyo kukosa ajira au kazi fulani bali ni
kutokujua ufanye nini kulingana na majira na nyakati unazoishi. Ni kutokuwa na hekima na ufahamu
ni pamoja na kuchukulia mambo kikawaida kawaida tu.
Kuna
umuhimu wa kujitambua katika nyakati tunazoishi kujua kuwa kuna mambo
muhimu ya kufanya na kuachana na mambo ya kipuuzi yasiyo na faida katika
maisha yetu.
Mtu anayejitambua atapangilia maisha
yake kulingana na muda alionao akiukomboa wakati kwa kufanya mambo yenye
tija na kuachana na yale yasiyo na maana au yenye kumpotezea muda kama
kukaa vijiweni, kumbi za starehe, kupoteza muda kwenye mitandao ya
kijamii, kutumia muda mwingi kwenye Tv na mambo yanayofanana na hayo.
Ndugu yangu na rafiki, ni
vyema kuukomboa wakati katika zama hizi tulizonazo na kuweka bidii
kwenye mambo muhimu katika maisha na kuepukana na umaskini ambao ni
janga kubwa sana linalotesa watu wengi sana duniani hivi leo.
Jitambue wewe ni nani, komboa wakati na utimize malengo yako ungali na nguvu, epuka kupoteza muda bali uutumie vizuri kwa faida.
Ni mimi rafiki yako
Innocent Moshi
0658 185 444/ 0625695550
E-mail: innommoja2@gmail.com
Comments
Post a Comment