NI KWA NINI MAONO YAKO HAYAFANIKIWI?
Ndugu
msomaji wa makala hii, huenda umewahi kujiuliza ni kwa nini unakuwa na maono lakini hayfanikiwi au hayatimii. Leo nataka tuzunguze kwa habari ya madhara yatokanayo na
kuwaambia watu maono uliyo nayo kabla ya kuyaweka katika vitendo.
Tutajifunza nini maana ya maono, faida ya kuwa na maono lakini pia
tutajifunza madhara yatokanayo na kuwaambia watu maono yako kabla
hayajatimia au hujayafanyia kazi.
Nini maana ya maono?
Yamkini umesikia hili neno maono lakini hujapata maana yake kamili.
Maono
ni picha ya mbeleni, malengo na mipango ambayo mtu anakuwa nayo na, ambayo atafanyia juhudi ili afikie au atimize. Malengo au mipango mtu
anaipanga kwa siku zijazo au wakati fulani ulioko mbeleni ili
kutekeleza, tunaweza kuichukulia kama maono mtu aliyo nayo.
Kwa
mfano, unataka baada ya miezi sita uwe na kiwanja cha kujenga nyumba au
uwe na gari lako mwenyewe, hayo ni maono ambayo unatamani yatimie
katika wakati huo. Hivyo tunaweza kusema kuwa hiyo ni picha yako ya
mbeleni uliyo nayo, ni malengo yako au ni mipango yako.
Kila
mtu ana jambo ambalo anafikiri katika maisha yake kwamba anatamani
kulitimiza labda ni mwaka mmoja au miwili au miezi kadhaa ijayo, kwa
kadiri ambavyo anataka mwenyewe na anafanya juhudi ili afikie hatima ya
maono yake. Kama unaishi bila malengo au bila mipango yoyote basi uko
katika hatari kubwa sana ya kutumbukia katika dimbwi la umaskini.
Mtu
mwenye akili timamu ni lazima afikiri kuhusu maisha yake ya baadae na
lazima awe na mikakati ambayo itamfikisha katika mafanikio ambayo
anatamani kuwa nayo.
Hakuna
jambo linaanza tu ghafla na kufanikiwa papo kwa hapo ila lazima mtu awe
amejiwekea malengo yake na kuanza kuyafanyia kazi taratibu hadi kufikia
hatua ya mafanikio.
Ni nini faida ya kuwa na maono?
Zipo faida zitokanazo na kuwa na maono ambazo nitazizungumzia hapa kwa uchache ila zipo nyingi zaidi ya hizi.
Kuwa na juhudi na kufanya kazi kwa bidii. Faida ya kuwa na maono ni kwamba yatakufanya uwe na juhudi kila siku ili uweze kuyatimiza na hii itakufanya usipoteze muda bure.
Kuwa na nidhamu ya fedha. Mtu mwenye maono ni lazima atakuwa na nidhamu ya fedha na kuepuka matumizi mabaya yasiyo na maana katika maisha yake. Kwa sababu anayo malengo anataka kuyatimiza, hivyo hataacha kutunza kipato chake alicho nacho au anachokipata ili kimsaidie katika kutimiza malengo yake.
Kutafuta kujifunza kwa watu sahihi. Mtu yeyote anayetaka kufanikiwa ni lazima atafute watu sahihi wa kujifunza kutoka kwao na siyo kila mtu. Japokuwa sikushauri kuwa uwaambie maono yako hata kama ni ndugu au rafiki zako wa karibu hata kama wamefanikiwa, lakini, kuna mambo unaweza kujifunza kwao pale unapokuwa nao na ukayatumia katika kutekeleza mipango yako. Kwa mfano, mbinu za kibiashara, mbinu za uzalishaji na mengineyo. Ukitaka kufanikiwa ishi na waliofanikiwa.
Utathamini muda wako. Kama una maono, hutokubali kupoteza muda bila sababu maana jinsi utakavyoupangilia muda wako ndivyo utakuwa na nafasi nzuri ya kusimamia mipango yako na ikafanikiwa kwa wakati sahihi.
Pamoja na kuwa kuna faida ya kuwa na maono, yapo madhara ya kuwaambia watu maono yako wakati bado hujayatimiza.
Watu
wanaweza kukwamisha maono yako. Ukiwaambia watu maono yako kuna hatari
kubwa sana ya kutokuyafikia kwa sababu yanaweza kukwamishwa na watu hao
hao unaowaambia kama hawana msaada kwako. Unaweza kumwambia mtu na
akakukatisha tamaa kama utakuwa unamtegemea akushauri na wakati wewe
ndiye mbeba maono.
Wanaweza kuyafanya wao kabla
wewe hujaanza. Kwa mfano una wazo la biashara fulani halafu ukawaambia
watu, pengine wana uwezo wa kuanza kutekeleza wakati wewe unatafuta pa
kuanzia, matokeo yake utaona wameshafanya na wewe ukija kuanza utakuwa
umechelewa.
Wanaweza kuyauwa bila wewe kujua. Siyo
watu wote wanapenda kuona mafanikio ya wengine. Ni vyema ukawa makini
sana na watu unaozungumza nao kwa habari ya maisha yako na mipango yako.
Siyo kila mtu anafaa kushirikisha maono yako. Wengine ni wauwaji wa
maono ya watu ili yao yafanikiwe.
Rafiki
yangu unayeasoma makala hii, Mungu akusaidie uweze kufikia malengo yako
na kutimiza maono yako kwa wakati muafaka, ila nakushauri uwe na
tahadhari sana usije ukatangaza maono yako kabla hujayafanyia kazi
kutokana na madhara ambayo umejifunza leo. Muhimu kuwa na maono maana
maisha bila kuwa na maono ni sawa na chombo kinachosafiri baharini bila
kiwa na dira (direction). Jitahidi sana uwe na dira ya kukuongoza katika
mafanikio yako.
Ni mimi rafiki yako
Innocent Moshi
0658 185 444/ 0625695550
E-mail: innommoja2@gmail.com
Kaka Asante kwa ushauri na maarifa yako
ReplyDeleteGood
ReplyDelete